Friday, May 16, 2014

Dengue yaingia Zanzibar, watatu wagundulika

Watu watatu wamelazwa katika Hospitali Kuuu ya Mnazimmoja mjini Zanzibar baada ya kushukiwa kuwa na maradhi ya homa ya Dengue inayosababishwa na mbu aina ya “Aedes”Ugonjwa huo tayari umeingia jijini Dar es Salaam na kuathiri watu zaidi ya 400 huku wengine wakiripotiwa
kufariki.Akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa, Waziri wa Afya, Juma Duni Haji, alisema, wagonjwa hao wametokea katika maeneo ya vijiji vya Kama na Mwera.Alisema, tokea wagonjwa hao wabainike, uongozi wa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja umeamua kuchukua vipimo kwa ajili ya kuvifanyia uchunguzi zaidi, ikiwa ni hatua ya kuweza kupata uthibitisho wa wagonjwa hao kama wanaugua homa hiyo.“Serikali kupitia Wizara ya Afya imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuchukua vipimo (Sample) ili kuchunguza kuwepo kwa virusi hivyo na kufuatilia sehemu walikotoka wagonjwa ili kutathmini hali halisi ya mazingira”, alisema Waziri huyo
Waziri Duni, alisema, wanalazimika kuchukua hatua hiyo kwa vile maradhi hayo ni mara ya kwanza kujitokeza hapa Zanzibar, hivyo ni vyema wananchi wakaona umuhimu wa kusafisha mazingira yanayowazunguka.Aidha, alifahamisha kuwa hadi sasa hakuna tiba maalum ya ugonjwa huo, na kwamba mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana kama vile homa, kupungukiwa na maji au damu huku akisisitiza hakuna chanjo kwa ajili ya kingaWaziri Duni, alisema katika kukabiliana na ugonjwa huo, serikali hivi sasa, inawasiliana na mashirika mbalimbali ya kimataifa ili yaweze kuwasaidia katika kuleta vifaa vya uuguzi kwa wagonjwa watakaopatwa na tatizo hilo.
Aliyataja mashirika ambayo wameanza kuwasiliana nayo ni pamoja na WHO, NIMR na Wizara ya Afya Tanzania Bara.
    Alizitaja dalili za ugonjwa huo ni homa ya hafla,mwili kuchoka, kuumwa na viungo, kuvimba tenzi na kupatwa na haraha (Vipele), kuumwa na kichwa ambapo dalili zake huanza kujitokeza kuanzia kati ya siku tatu na 14 tangu mtu alipoambukizwa.
“Dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria na homa ya mafua, hivyo nawaomba wananchi kuwa waangalifu hasa wakati wanapopata homa ambazo zinafanana na malaria kukimbilia vituo vya afya,” alisema.
Hata hivyo, alifahamisha kuwa kuna aina tofauti za ugonjwa huo, ikiwemo (Dengue Fever) ambapo huambatana na dalili kuu tatu za homa kali ghafla, kuumwa kichwa na maumivu ya viungo au uchovu.
Dk. Salma Masauni Yussuf, ambae ni Mkuu wa Kitengo cha kuzuia na kudhibiti maradhi Zanzibar, aliwataka wananchi kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha hali inakuwa nzuri hapa nchini huku akiwanasahi kusafisha mazingira hasa katika kipindi hichi cha mvua za masika zinazoendelea.

No comments:

Post a Comment