Thursday, April 24, 2014

Gari la kisasa la matangazo la TBC

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), limepatiwa gari jipya la kisasa la kurushia matangazo ya nje (OB Van), ambalo kwa mara ya kwanza litatumiwa kwenye matangazo ya sherehe za miaka. 50 ya Muungano wa Tanzania kesho kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Gari hilo kutoka Serikali ya China limeshawasili na tayari mafundi tisa wa Kichina wapo nchini ili kusaidia katika urushaji wa matangazo hayo ya sherehe za Muungano pamoja na kuendesha mafunzo kwa mafundi wa TBC.Kundi la mafundi wa TBC lilikwenda China wiki chache zilizopita kujifunza jinsi ya kutumia gari hilo ambalo limeelezwa kuwa bora kwa kurushia matangazo ya televisheni ya nje kuliko jingine lolote hapa nchini kwa sasa.Ofisa mwandamizi wa TBC1 ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema ili kukidhi matakwa ya matumizi ya gari hilo, shirika lao limewajibika kununua gari jingine jipya (pick up) lenye thamani ya Sh60 milioni kwa ajili ya kubebea mtambo rasmi wa gari hilo wa kurushia matangazo yake hayo.Alisema sherehe rasmi za uzinduzi na makabidhiano ya gari hilo zitafanywa baada ya kumalizika kwa shughuli za sherehe za Muungano.

No comments:

Post a Comment